 |
| Mbwa mwitu wakila nyama |
Rais Jakaya Mrisho Kikwete ameishukuru kampuni ya simu za mkononi ya
Vodacom kwa kuchangia katika mradi wa kuhifadhi mbwa mwitu katika
hifadhi ya Taifa ya Serengeti, mradi unaojulikana kama Vodacom
Foundation Serengeti Wild Dogs Conservation Project, kwa dola za
Marekani 450,000 kwa kipindi cha miaka mitatu.
Rais ametoa shukrani hizo Kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom hapa nchini
Bw. Rene Meza, Ikulu Dar-Es-Salaam, walipokutana jana jioni, Ijumaa
Agosti 31,2012
"Napenda kutoa shukrani zangu kwa Vodacom kwa msaada huu mkubwa, tunashukuru kwa jitihada zenu kubwa katika hili" Rais amesema.
Naye Mtendaji Mkuu wa Vodacom amemhakikishia Rais kuwa kampuni yake
itaendelea kushirikiana na serikali katika miradi mbalimbali ya
maendeleo, elimu na Afya.
“Tunajisikia faraja sana kuwa
miongoni mwa washirika wa mradi huu. Ni heshima kwetu na tuko makini
nao, tunataka kuendelea na mradi huu" Bw, Rene Meza amemhakikishia Rais.
Tayari mbwa mwitu kumi na Moja,
wamerudishwa mbugani siku ya Alhamisi Agosti 30, 2012 baada ya
kuhifadhiwa kwenye boma maalumu la mradi huo, katika eneo la Nyamuma,
Magharibi mwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, mkoani Mara.
Wadau
wengine walioshiriki na kufanikisha zoezi hilo ni pamoja na Idara ya
Wanyamapori, Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), Mamlaka ya Hifadhi ya
Ngorongoro (NCCA), Frankfurt Zoological Society, Grumeti Fund na
Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro.
Kuachiwa
kwa Mbwa Mwitu hao 11 walioondolewa katika msitu wa Samunge wilayani
Loliondo ni mojawapo ya juhudi za kurudisha tena makundi ya wanyama hao
katika mbuga hiyo maarufu duniani. Hivi sasa kuna makundi 11
yanayofuatiliwa, manane yakiwa Loliondo na matatu katika Hifadhi ya
Ngorongoro, yakifanya jumla ya Mbwa Mwitu 200.
Mtafiti wa
Magonjwa ya Wanyama kutoka Taasisi ya Utafiti wa Wanyama (TAWIRI) Dkt.
Ernest Mjingo, alimwambia Rais Kikwete kwamba katika Hifadhi ya
Serengeti makundi ya Mbwa Mwitu yalikuwa yakionekana kwa wingi, lakini
sasa yametoweka na mara ya mwisho Mbwa Mwitu wawili walionekana mwaka
1998.
Mtafiti huyo alisema Mbwa Mwitu wamekuwa wakitoweka
kutokana na kuuawa kwa sumu na wananchi baada ya kula mifugo yao na
kuugua magonjwa mbalimbali kama kichaa cha mbwa.
Dkt. Mjingo
alisema baada ya kuachiwa Mbwa Mwitu hao, waliovishwa collar maalumu
zenye redio, juhudi zitaendelea ili kupata makundi sita yenye Mbwa
Mwitu takriban kumi kila moja, ikiwa ni hatua endelevu ya muda mrefu ya
kuhakikisha uwepo wa wanyama hao mbugani humo.
Mbwa Mwitu ni
miongoni mwa wanyamapori ambao wapo hatarini kutoweka duniani. Takwimu
zinaonyesha kuwa katika Bara la Afrika kuna Mbwa Mwitu wanaofikia 8,000
na Tanzania pekee inakadiriwa kuwa wanyama hao 3,500 katika mbuga
mbalimbali nchini. Katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti walitoweka
kabisa kabla ya juhudi hizi za kuwarejesha kuanza.