Monday, July 23, 2012

BENKI YA POSTA YATOA MILIONI 5 KWA AJILI YA URATIBU WA KONGAMANO LA KUJADILI MASUALA YA UTALII

Kongamano la kujadili masuala ya utalii kwenye nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania linatarajia kufanyika Agosti 8 na 9, mwaka huu kisiwani Zanzibar ikiwa ni sehemu ya mpango mkakati wa kukuza sekta ya utalii nchini.

Kongamano hilo linatarajia kushirikisha wadau mbalimbali wa sekta ya utalii wakiwemo wanataaluma na watunga sera ili kujadili mbinu za kutafuta masoko na kukabili changamoto zilizopo kwenye sekta ya utalii.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Posta Tanzania Sabasaba Moshingi amesema kuwa bado jitihada za ziada zinahitajika katika kukuza sekta ya utalii nchini ikiwa ni pamoja na kutafuta masoko kwenye sekta hiyo.

Moshingi amesema hayo wakati akikabidhi hundi ya Shilingi milioni tano kwa Idara ya Masoko ya Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam kwa ajili ya uratibu wa kongamano hilo.

Akipokea hundi hiyo Mkuu wa Idara ya Masoko wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dr Lufumbi Mwaipopo anataja mambo yatakayojadiliwa katika kongamano hilo.

Amesema umefika wakati kwa watanzania kuendeleza sekta ya utalii bila kutegemea wafadhili kutokana na kutohitaji fedha nyingi kwa ajili ya uwekezaji.

Kongamano ni sehemu ya mpango mkakati wa upatikanaji wa mbinu za kuimarisha sekta ya utalii nchini ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa sera zitakazosaidia kupanua wigo wa sekta hiyo na ongezeko la watalii nchini.

No comments:

Post a Comment